22 Juni 2026 - 23:16
Pakistan: Ziara ya Rais Pezeshkian Islamabad Yaakisi Dhamira ya Pamoja ya Amani na Maendeleo ya Kikanda

Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imesema ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, nchini Pakistan inaonesha azma ya pamoja ya Tehran na Islamabad ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kitamaduni, pamoja na kuendeleza amani, utulivu na maendeleo endelevu katika eneo.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imetangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, anatarajiwa kuwasili Islamabad Jumanne, tarehe 23 Juni 2026, kwa ziara rasmi kufuatia mwaliko wa Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif.
 
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Wizara hiyo ilieleza kuwa ziara hiyo inaakisi dhamira ya pamoja ya Iran na Pakistan ya kuimarisha zaidi uhusiano wao wa muda mrefu unaojengwa juu ya misingi ya historia, utamaduni na ujirani mwema.
 
Taarifa hiyo imebainisha kuwa nchi hizo mbili zina matarajio yanayofanana kuhusu kuimarisha amani, utulivu na maendeleo endelevu katika eneo, huku zikilenga pia kupanua ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na kiusalama.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi wa Iran na Pakistan wanatarajiwa kujadili masuala muhimu ya pande mbili, pamoja na maendeleo ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja kwa mataifa hayo mawili.
 
Ziara ya Rais Pezeshkian nchini Pakistan inafanyika katika kipindi ambacho Tehran na Islamabad zinaendelea kuonyesha nia ya kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati, sambamba na juhudi za kukuza uthabiti, usalama na maendeleo katika eneo la Asia Kusini na Mashariki ya Kati.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha